Mshambuliaji wa timu ya Yanga, Hamis Tambwe.
INGAWA Simba bado ni ya mwendokasi katika kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini benchi la ufundi haliridhishwi na kiwango cha safu ya ushambuliaji kwani wameendelea kutegemea nguvu ya safu ya kiungo kusaka pointi tatu, tofauti na Yanga ambao washambuliaji wake chini ya Amissi Tambwe wanafanya vizuri. Ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Ndanda uliwarejesha kileleni Wekundu wa Msimbazi kwa pointi 38, pointi mbili mbele ya Yanga kwa mabao ya viungo Mzamiru Yassin na Mohammed Ibrahim ‘Cabaye’ lakini benchi hilo linaona kuwa wana kazi kubwa ya kufanya.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ‘Mia Mia’, amesema hawafurahishwi na mwenendo wa mafowadi wao kwani hakuna aliye juu kwenye chati ya ufungaji zaidi ya kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya anayeongoza kwa mabao tisa sawa na Simon Msuva wa Yanga. Katika chati hiyo, Tambwe anawafuatia kwa mabao saba sawa na fowadi Rashid Mandawa wa Mtibwa Sugar huku fowadi tegemeo wa Simba, Fredric Blagnon akiwa amefunga bao moja, Ibrahim Ajibu ‘Cadabra’ ana mabao matatu na Laudit Mavugo amefunga matano tu. “Huwezi kufurahia kama unaona kwenye chati ya juu hakuna straika wako, hakuna mwenye mabao saba kulinganisha na wengine kama Kichuya na Tambwe kwenye chati ya wafungaji.
“Angalia ni mechi ngapi hakuna straika wetu amefunga bao? Kweli ni jambo ambalo bado kama benchi la ufundi linatuumiza akili na ndiyo maana utaona tunafanya kila jitihada kuhakikisha tunaiboresha safu ya mbele kama wenzetu. “Hiyo ni tofauti na Yanga kwani Tambwe mara ya mwisho alifunga mechi tatu zilizopita, raundi ya 13 wakati wakiichapa Mbao mabao 3-0 kabla ya Donald Ngoma kufunga raundi ya 14 kwenye kichapo cha mabao 2-1 mechi dhidi ya Mbeya City ugenini, hawa wanatufanya tuumize sana kichwa kwa kuwa mabao mara nyingi yanafungwa na viungo.”